Mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona wameandika historia ya kuwa klabu ya kwanza barani Ulaya kwa kupindua mlima wa mabao kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani humo.
FC Barcelona walikua nyuma kwa mabao manne dhidi ya PSG na mashabiki wengi ulimwenguni kote walitarajia kuona wakitupwa nje ya michuano hiyo, kwani haikuwahi kutokea miaka ya nyuma kwa klabu kugeuza matokeo kutoka mabao manne.
FC Barcelona walitakiwa kupata ushindi wa mabao matano kwa sifuri na kuendelea ili wafanikiwe kupita kwenye hatua ya 16 bora, jambo ambalo lilifanikiwa kwa kupata ushindi wa zaidi ya kiasi hicho cha mabao.
Katika mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa Camp Nou usiku wa kumakia leo, ulishuhudia FC Barcelona wakichomoza na ushindi wa mabao sita kwa moja, ambao umewawezesha kusonga mbele kwa jumla ya mabao sita kwa matano.
Mabao ya FC Barcelona dhidi ya PSG usiku wa kuamkia leo, yalifungwa na Luis Suarez, Lionel Messi, Neymar alifunga mabao mawili, Sergi Roberto na Layvin Kurzawa aliyejifunga mwenyewe.