Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imejipanga kuitangaza Tanzania kama eneo bora la utalii katika maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yajulikanayo kama Internationalle Tourismus Borse (ITB) yaliyoanza rasmi jijini Berlin Ujerumani katika eneo la Messe Berlin na kuhudhuriwa na jumla ya nchi 187 kutoka kote duniani.
Hayo yamesemwa na Meneja Masoko wa Bodi ya TTB, Geofrey Meena, amesema kuwa TTB imejipanga kuitangaza Tanzania kama eneo bora la utalii duniani ambapo pamoja na kuendelea kuvitangaza vivutio kama vile mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro, Hifadhi za Taifa, fukwe na maeneo mbalimbali ya kihistoria.
Aidha, amesema mwaka huu mkazo umewekwa katika kutangaza ushahidi wa nyayo za binadamu wa kale (Zamadamu) uliovumbuliwa miaka milioni nne iliyopita katika eneo la Laetoli lililoko takribani kilometa 45 kusini mwa Olduvai Gorge.
“Pamoja na kuvumbuliwa kwa fuvu la anayesadikiwa kuwa ni binadamu wa kwanza kabisa duniani huko Olduvai Gorge Ngorongoro, lakini katika kuendelea kudhihirisha kuwa Binadamu wa kwanza aliishi Tanzania tumeamua katika maonesho ya mwaka huu kuja na ushahidi unaoelezea ukweli huo kwamba Binadamu asili yake ni Tanzania,” amesema Meena.