Beki wa kati wa klabu ya Simba, Method Mwanjali ataendelea kuwa nje kwa mwezi wote wa Machi kutokana na maumivu ya goti.
Mwanjali ambaye ni raia wa Zimbabwe hajajumuishwa kwenye kikosi kilichoondoka leo Dar es Salaam kwenda ziara ya Dodoma kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji, Polisi – Dodoma Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe amesema Mwanjali hayupo kwenye msafara wa kwenda Dodoma na hatahusishwa kwenye programu yoyote ya timu mwezi huu wa Machi.
Gembe amesema wanataka Mwanjali aendelee kupatiwa matibabu hadi awe fiti kabisa, ili akirejea iwe amerudi rasmi kuisaidia timu.
“Tunataka apone vizuri kabisa ndiyo arejee uwanjani. Kwahiyo, Machi yote hatakuwemo kwenye programu za timu,”amesema Gembe.
Mwanjali aliumia goti katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons Februari 11, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ikishinda 3-0.
Mchezaji huyo aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alitolewa kwa machela siku hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na kizungu, Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 62.