Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), limetoa siku 14 kwa Wateja wake wote wanaodaiwa
kulipa madeni yao, vinginevyo litasitisha utoaji wa huduma ya nishati kwa wahusika.
Akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa Habari mapema hii leo Ofisini kwake Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dkt. Tito Mwinuka, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania Tanesco linadai jumla ya sh. Bilioni 275.38.
Amesema kuwa, Wizara na Taasisi za Serikali zinadaiwa zaidi ya Sh. bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO), linadaiwa zaidi ya Sh. Bilioni 127.87, na Makampuni binafsi na wateja wadogo wadogo deni ni zaidi ya Sh.bilioni 94.97.
“Zoezi hili litaambatana na utoaji taarifa kwa wadaiwa wote kulipa madeni yao ndani ya kipindi cha siku 14, baada ya hapo Shirika litachukua hatua ya kusitisha Huduma kwa Wateja watakaoshindwa kuanza kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria.” amesema Dkt. Mwinuka.
Aidha, amesema kuwa kwa wale wateja wadogo wadogo, Shirika halitawaandikia barua kwani ni
wengi, isipokuwa kupitia Ofisi ya Uhusiano ya Shirika, watataarifiwa kupitia vyombo vya habari
Hata hivyo, Taarifa hiyo ya Tanesco imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, kuliagiza Shirika hilo, kuwakatia umeme wale wote wanaodaiwa zikiwemo
taasisi nyeti za Serikali na hata Zanzibar.