Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajia kukutana leo Brussels katika mkutano wa kilele uliogubikwa na ajenda kadhaa ikiwemo suala la uchaguzi wa Rais wa Baraza la hilo.
Mkutano huo pia unatarajia kuzungumzia masuala mengine ikiwa ni pamoja na suala linalohusiana na uchumi barani ulaya, hali ya sasa ya ukanda wa magharibi wa nchi za Balkan pamoja na suala la ulinzi na ushirikiano wa kijeshi.
Aidha, mkutano huo huenda ukawa wa mwisho kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana kabla ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, kuanzisha rasmi mchakato wa kujitoa kwenye umoja huo kwa kutumia ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon.
Uingereza inatarajia kutangaza rasmi kusudio lake la kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi na hivyo kuanza rasmi kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Mkutano huo unafanyika wakati kukiwa na mvutano kati ya Waziri Mkuu wa Poland Beata Szydlo na viongozi wengine wa mataifa yanayounda umoja huo.