Beki wa kulia kutoka nchini Ufaransa Bacary Sagna amepania kuondoka Man City na kurejea jijini London kujiunga na wagonga nyundo wa jiji hilo West Ham Utd.
Meneja wa West Ham Utd Slaven Bilic, amedhamiria kufanya maboresho ya upande wa ulinzi wa kulia wa kikosi chake, baada ya kuona changamoto hiyo ikimkabili msimu huu.
Bilic amedhamiria kuboresha eneo hilo, kwa kutumia mwanya wa kumpata kirahisi Bacary Sagna ambaye atakuwa huru mwishoni mwa msimu huu, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwezi Juni.
Sagna, mwenye umri wa miaka 34, bado hajafahamu kama atapewa mkataba mpya ama la, jambo ambalo linaendelea kuiweka rehani hatma yake ndani ya kikosi cha Guardiola.
Sagna, ambaye anapokea mshahara wa Pauni 60,000 kwa juma, anaona njia pekee ya kunusuru soka lake ni kurejea jijini London ambapo aliishi huko kwa miaka saba akiwa na klabu ya Arsenal kabla ya kuondoka mwaka 2014.
Nafasi ya beki wa kulia katika kikosi cha West Ham Utd inatumikiwa na Cheikhou Kouyate ambaye ameonyesha kushindwa kuimudu, baada ya Sam Bryam aliyesajiliwa akitokea Leeds Utd kukabiliwa na majeraha ya muda mrefu.
Kwa asili Cheikhou Kouyate ambaye ni raia wa Senegal ni mchezaji anapendelea kucheza nafasi ya kiungo, na alilazimishwa kucheza nafasi ya beki wa kulia kutokana na changamoto zilizopo West Ham Utd.