Kiungo kutoka nchini Croatia Ivan Rakitic amekubali kusaini mkataba mpya na klabu ya Barcelona ya Hispania, ambao utamuwezesha kuwepo Camp Nou hadi mwaka 2021.
Rakitic amekamilisha mpango huo, baada ya kuhusishwa na taarifa za muda mrefu za kutaka kusajiliwa na klabu za nchini England, na ilifikia hatua ada yake ya usajili ilitajwa kufikia zaidi ya Pauni milioni 100.
Klabu pinzani za mjini Manchester zilihusishwa katika taarifa za kumuwania mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huu, lakini kwa sasa hazina namna ya kumsaka mbadala wake, kama kweli walikua wakimuhitaji kiungo huyo mchezeshaji.
Taarifa rasmi zilizotolewa na FC Barcelona zimeeleza kuwa, tukio la kusaini mkataba mpya kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28, litafanyika baadae hii leo mjini Barcelona.
Rakitic alisajiliwa na FC Barcelona mwaka 2014 akitokea Sevilla CF, na tayari ameshaitumikia klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Hispania katika michezo ya 145 na kufunga mabao 23.