Shinikizo la baadhi ya mashabiki wa klabu ya Arsenal la kutaka meneja wa klabu hiyo asipewe mkataba mpya, huenda likawa kazi bure kutokana na uongozi wa juu kuonyesha kuwa pamoja na Arsene Wenger.

Mwenyekiti wa The Gunners Sir Chips Keswick, amekiri bado wapo sambamba na meneja huyo kutoka Ufaransa, na maamuzi ya kutosaini ama kusaini mkataba mpya yataamuliwa na bodi.

Keswick amezungumza kwa mara ya kwanza tangu shinikizo hilo lilipokolezwa na matokeo mabovu yanayokiandama kikosi cha Arsenal siku za karibuni, ambapo amesema ni kazi ya bodi kuamua nani anapaswa kuwa meneja wa kikosi, na sio kundi la watu wachache.

Amesema wanatambua mkataba wa Wenger utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, na taratibu wa kumpa mkataba mpya ama kumsaka mbadala wake zitaanza kuchukua nafasi wakati wowote kuanzia sasa.

Keswick amesema:  “Tupo makini katika suala hilo, hatutaki kuamuliwa na mtu yoyote zaidi ya kuheshimu vikao vya bodi na maamuzi yatakayochukuliwa.

“Tunawaheshimu mashabiki wetu duniani kote, na tunajua namna wanavyochukizwa na kinachoendelea uwanjani, lakini hatuna budi kuheshimu nafasi ya meneja aliyonayo kwa sasa kutokana na mkataba uliopo.

“Arsène bado ana mkataba hadi mwishoni mwa msimu huu. Mimi pamoja na viongozi wa bodi tunajua tutakachokifanya tena kwa wakati maalum, na kwa njia sahihi.”

Wenger mwenye umri wa miaka 67, amekua meneja wa kikosi cha Arsenal tangu mwaka 1996.

Kamati Ya Nidhamu Yaiagiza TFF
Pep Guardiola Kumvuta Dani Alves