Kwa mara ya kwanza kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet amezungumzia kilichomsukuma kuihama West Ham Utd wakati wa majira ya baridi (Mwezi Januari).
Payet alijiunga na Olympic Marseille kwa dau la Pauni milioni 25, baada ya kukabiliwa changamoto kadhaa kutoka wa wachezaji wenzake kufuatia maamuzi ya kutaka kuondoka ambayo aliyatangaza hadharani tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Kiungo huyo ambaye alionyesha soka safi msimu uliopita akiwa na West ham Utd, amefichua siri hiyo alipohojiwa na gazeti la L’Equipe, ambapo amesema alianza kushawishika kuondoka klabuni hapo baada ya kuchoshwa na mbinu za meneja Slaven Bilic.
Amesema mbinu za meneja huyo kutoka nchini Croatia zilikua kikwazo kikubwa kwa West Ham Utd kufanya vizuri katika michezo ya mwanzo wa msimu huu, na aliona hakuna haja ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo ambayo ilikua imepoteza muelekeo wa kushindana.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 ambaye tayari ameshafunga mabao matatu katika michezo minane aliyocheza tangu aliposajiliwa na Olympic Marseille mwezi Januari mwaka huu, amesema mara kadhaa alidiriki kumshauri Bilic kubadili mfumo na kutumia ule wa msimu uliopita lakini ilikua ngumu kueleweka.
‘Sikufurahishwa na maamuzi ambayo meneja aliamini ni sahihi bila kujali hisia za watu wengine, nilishiriki mara kadhaa kumpa ushauri lakini alinipuuza, na matokeo yake yalikua yakionekana uwanjani,
‘Nililazimika kubadili mawazo yangu na kushinikiza suala la kuihama West ham Utd, lakini bado suala hilo liliniletea matatizo makubwa hadi kufikia hatua ya kutengwa na wachezaji wenzangu, lakini kumbuka, yote haya yalisababishwa na ukweli niliousema kama ushauri wa kurejea kwenye njia sahihi ya ushindi.”
Kuhusu maisha ya Ufaransa tangu aliporejea nchini humo mwezi Januari, Payet amesema anayafurahia na amekua na ushirikiano mzuri na wachezaji wengine wa Olympic Marseille, jambo ambalo linampa nafasi ya kucheza kwa uhuru na kufunga mabao.
Kabla ya kujiunga na West Ham Utd Payet alikua akiitumikia Olympic Marseille tangu mwaka 2013 hadi 2015 ambapo alicheza michezo 72 na kufunga mabao 15.
Akiwa na West Ham Utd kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 alicheza michezo 48 na kufunga mabao 11.
Klabu nyingine ambazo Payet amewahi kuzitumikia ni AS Excelsior (2004–2005) michezo 36 mabao 12, Nantes (2005–2007) michezo 33 mabao 5, Saint-Étienne (2007–2011) michezo 129 mabao 19, Lille 71 (2011–2013) michezo 71 mabao 18.