Wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mbunge mmoja, wanahojiwa na Jeshi la Polisi Mjini Dodoma kwa madai ya kutaka kufanya uchochezi na Vurugu katika vikao vya CCM vinavyoendelea Mjini humo.
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa amethibitisha kukamatwa kwa wanachama watatu wa CCM kwa madai ya kufanya vurugu kwenye vikao vya CCM vinaendelea mjini Dodoma.
Mambosasa amewataja waliokamatwa ni pamoja na Mjumbe wa NEC, Adam Malima, Husein Bashe ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini na Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma ambaye ni Mbunge wa Geita vijijini.
“Tunawashikilia si kwa sababu ya kutaka kupigana kwenye kikao, ila kwa kufanya uchochezi na vurugu katika vikao vya CCM,”amesema Mambosasa.
Hata hivyo, baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho wametoka hadharani katika kikao hicho na kutangaza kujitenga na Kamati ya Usalama na Maadili kwa kupeleka majina matano kwenye CC badala ya wagombea wote kama kanuni zinavyoeleza.