Mabingwa wa soka nchini Ujerumani, Klabu ya Bayern Munich huenda wakaanzisha ugomvi na klabu ya Arsenal, kufuatia taarifa zilizotolewa na aliyekuwa meneja wao, Ottmar Hitzfeld  kuhusu kiungo Granit Xhaka.

Hitzfeld amehojiwa na gazeti la Bild na kueleza wazi mipango inayosukwa na mabingwa hao wa Ujerumani, kuhusu kiungo  Xhaka ili aweze kurejea katika ligi ya Bundesliga.

Meneja huyo mkongwe ambaye pia aliwahi kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Uswiz, ameliambia gazeti hilo kuwa ana uhakika wa kutosha kuhusu mpango huo ambao unaandaliwa kukamilishwa mwishoni mwa msimu huu.

Arsenal walimsajili Xhaka akitokea Borussia Mönchengladbach mwishoni mwa msimu uliopita na aliwagharimu washika bunduki hao kiasi cha Pauni milioni 35.

Taarifa za kusukiwa mipango na uongozi wa FC Bayern Munich huenda zikaibua zogo dhidi ya viongozi wa Arsenal kupitia meneja Arsene Wenger, ambaye inaaminika hatokubali kirahisi kumuachia kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24.

Xhaka amekuwa akipambana vilivyo katika nafasi ya kiungo mkabaji, licha ya kukabiliwa na adhabu za kadi nyekundu tangu alipojiunga na The Gunners. Jambo hilo huenda likawa sababu kubwa ya uhamisho wake kuibua zogo.

Kadhalika, Arsenal ipo katika hatari ya kuwapoteza wachezaji wengine mwishoni mwa msimu huu kama mshambuliaji kutoka Chile, Alexis Sanchez ambaye ameripotiwa kutokuwa na mahusiano mazuri na mchezaji wenzake, Mesut Ozil ambaye ameshindwa kuonyesha dalili za kusaini mkataba mpya  licha ya kuahidiwa kupewa mshahara wa Pauni 280,000 kwa juma.

Mwingine ni kiungo mshambuliaji, Alex Oxlade-Chamberlain ambaye tayari baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa hapendezwi na mbinu za ufundishaji za mzee Wenger.

RasenBallsport Leipzig Kuja na taarifa kamili ya Naby Keita
Pigo Man Utd, Kupambana Bila Mshambuliaji