Kiungo Naby Keita anayefikiriwa huenda akaziingiza vitani klabu za Liverpool na Arsenal katika soko la usajili mwishoni mwa msimu huu, mwishoni mwa juma alikimbizwa hospitali baada ya kupoteza fahamu akiwa uwanjani katika mchezo wa ligi ya nchini Ujerumani kati ya RasenBallsport Leipzig dhidi ya Wolfsburg.
Keita alipoteza fahamu baada ya kucheza dakika 90 za mchezo huo, na sekunde chache baadae alilazimika kukimbizwa hospitali kutokana na mwili wake kukosa nguvu, hali iliyosababisha apoteze fahamu.
Taarifa zilizotolewa na klabu yake ya RasenBallsport Leipzig zimeeleza kuwa alipofikishwa hospitalini, hali yake ilifanikiwa kurejea na alipatiwa matibabu kwa saa kadhaa.
Hata hivyo, uongozi wa klabu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya nchini Ujerumani kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara FC Bayern Munich, umeahidi kutoa taarifa kamili kuhusu Keita siku kadhaa zijazo.
Keita amekuwa na msimu mzuri, jambo ambalo limeongeza ushindani wa saini yake kusakwa kwa udi na uvumba. Tayari meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp ameripotiwa kutenga kiasi cha Pauni milioni 30 kwa ajili ya kumnyakua.
Klabu nyingine ya England inayotajwa kumuwania kiungo huyo kutoka Guinea ni Arsenal ya kaskazini mwa jijini London, lakini bado haijaelelezwa imetenga kiasi cha Pauni ngapi ili kufanikisha mpango huo.
Klabu nyingine zinazoripotiwa kumuwania Keita ni FC Bayern Munich, Borussia Dortmund na Atletico Madrid.
Keita alijiunga na RasenBallsport Leipzig mwezi Juni mwaka 2016, akitokea nchini Uswiz alipokuwa akiitumikia klabu ya Red Bull Salzburg.