Klabu ya Man Utd imeutema rasmi ubingwa wa kombe la FA baada ya kukubali kichapo cha bao moja kwa sifuri, kutoka kwa vinara wa ligi kuu ya soka nchini England, Chelsea.
Man utd walisafiri hadi jijini London kucheza mchezo huo wa hatua ya robo fainali, na walijikuta wakiruhusu bao hilo pekee katika dakika ya 51 ambalo lilifungwa na kiungo N’Golo Kante.
Man Utd walicheza kwa kipindi kirefu wakiwa pungufu, kufuatia kiungo wao kutoka nchini Hispania, Ander Herera kuoneshwa kadi ya njano mara mbili na kisha kadi nyekundu katika dakika ya 35.
Herera alikumbana na adhabu hiyo baada ya kumchezea rafu kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Eden Hazard na kusababisha mchezo kubadilika na kuwawezesha wenyeji kucheza kwa kujiamini wakati wote.
Mbali na tukio hilo la adhabu ya kadi nyekundu, Mchezo huo ulighubikwa na matukio yatokanayo na hasira. Mshambuliaji wa Chelsea, Diego Costa na beki wa Man Utd, Marcos Rojo walizozana mara kwa mara huku meneja Antonio Conte akikwaruzana na Jose Mourinho.
Marcus Rashford, ambaye wengi hawakutarajia angecheza kwa kuwa alikuwa mgonjwa, alipata nafasi nzuri ya kusawazisha goli, lakini kipa wa Chelsea Thibault Courtois alizuia mkwaju wake.
Matokeo ya mchezo huo wa kombe la FA, yanaendelea kumuweka katika hali ya simanzi meneja wa Man Utd, Jose Mourinho ambaye amekubali kupoteza kwa mara ya pili dhidi ya waajiri wake wa zamani.
Kwa mara ya kwanza Mourinho alipoteza mchezo dhidi ya Chelsea katika mpambano wa ligi ya England uliochezwa mwezi Oktoba mwaka jana, kwa kukishuhudia kikosi cha Man Utd kikikubali kibano cha mabao manne kwa sifuri.