Rais wa shirikisho la soka nchini Liberia, Musa Bility amesema Afrika inapaswa kuwa katika mabadiliko makubwa kisoka kupitia uchaguzi mkuu wa shirikisho la mchezo huo Afrika (CAF).

Bility amezungumza suala hilo alipohojiwa na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), kuelekea katika uchanguzi mkuu wa CAF, ambao umepangwa kufanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Machi 16 mwaka huu.

Bility ameeleza jinsi alivyodhamiria kuhakikisha kura yake inakwenda kwa mgombea Ahmad Ahmad, ambaye ni mpinzani wa Rais wa sasa wa CAF, Issa Hayatou.

Amesema umefika wakati wa kulitazama bara la Afrika kwa upana wa mabadiliko, na sio kuangalia sura ya mtu kwa kigezo cha kukaa madarakani kwa muda mrefu.

“Afrika inapaswa kubadilika kwa kuwa na kiongozi atakaeleta changamoto mpya za kiuongozi, ninaeleza wazi bila kificho Hayatou anastahili kupumzika baada ya kuwa kiongozi wa soka la bara hili kwa kipindi kirefu,” alisema Bility.

Issa Hayatou amekuwa madarakani tangu mwaka 1988, na mwaka huu anawania kiti cha urais kwa mara ya nane mfululizo.

Alexis Sanchez Kumpeleka Karim Benzema Emirates Stadium
Hassan Kabunda Mchezaji Bora Februari