Kiungo kutoka nchini Ujerumani, Emre Can amethibitisha kuwa katika mpango wa kurejea kwenye mzungumzo ya kusaini mkataba mpya, ambao huenda ukamuwezesha kubaki na majogoo wa jiji (Liverpool).

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, alisitisha mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo, kwa kigezo cha kutoridhishwa na kiwango cha mshahara, ambacho kilipendekezwa kwenye mkataba wake mpya.

Can ameiambia tovuti ya Liverpool kuwa hana budi kurejea mezani na kufanya upya mazungumzo na uongozi, baada ya kuona hakuna haja ya kuendelea kusubiri, kutokana na jambo hilo kuwa na umuhimu mkubwa katika maisha yake.

Amesema kuna baadhi ya vyombo vya habari vimelibeba suala hilo la kukataa kuendelea na mazungumzo ya kusaini mkataba mpya kama fimbo ya kumchapia, na wakati mwingine vinamtuhumu kwa kumuita mpenda pesa.

“Nimesoma baadhi ya magazeti, nimeona jambo hilo lilivyochukuliwa tofauti, sikuwa na maana mbaya kwa kukataa kuendelea na mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, bali nilizingatia mambo ya msingi,” amesema Can.

“Tulifikia pazuri na viongozi wangu, lakini nilipendekeza suala la maslahi liangaliwe upya kutokana na uzito wa majukumu nilionayo hapa, inafahamika ninapambana sana kwa kushirikiana na wenzangu, na kama klabu imeona kuna haja ya kuendelea kuwepo hapa, bado suala la maslahi yangu nilitaka liangaliwe upya,” aliongeza.

Emre Can alisajiliwa na Liverpool mwaka 2014 akitokea nchini Ujerumani alipokua akiitumikia klabu ya Bayer Leverkusen, na mpaka sasa ameshaitumikia The Reds katika michezo 79 na kufunga mabao 6.

Yaya Toure Atuma Salamu Kwa Wasioipenda Man City
Alexis Sanchez Kumpeleka Karim Benzema Emirates Stadium