Kiungo wa Man City, Yaya Toure amewashukia baadhi ya mashabiki wa soka nchini England na pengine ulimwenguni, ambao wanasubiri kuona klabu hiyo ikishindwa kutinga katika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Toure amesema watu hao wapo, na wanatarajia kuona kikosi cha Guardiola kikishindwa dhidi ya AS Monaco kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa 16 bora ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, utakaochezwa kesho mjini Monaco nchini Ufaransa.
Kiungo huyo kutoka nchini Ivory Coast amesema huenda watu hao wakawa na mawazo ya kutaka City wapoteze kutokana na chuki zao binafsi, lakini akawakumbusha kuhusu dakika 90 ambazo zitaamua nani atasonga mbele na nani atabaki.
“Mchezo wa soka una matokeo, na kesho ni lazima mmoja kati ya Man City ama AS Monaco atabaki na mwingine ataendelea na mashindano, tusubiri dakika 90 ama zaidi, ili kuona nani atafanikiwa,” anakaririwa.
“Hainiingii akilini kwa kundi la watu kutaka timu ifungwe wakati mchezo haujachezwa, ninawashauri ni bora wakasubiri kwanza na kuona nani atakuwa na uwezo mzuri wa kumshinda mwingine,” aliongeza kiungo huyo alipohojiwa na tovuti ya Tribalfootball.
Man City wamesafiri kuelekea mjini Monaco nchini Ufaransa huku wakiwa na mtaji wa mabao matano kwa matatu, na kama watahitaji kusonga mbele watatakiwa kulinda walichokipata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, ambao ulichezwa mjini Manchester majuma mawili yaliyopita.
Njia nyingine kwa klabu hiyo kusonga mbele na kutinga kwenye hatua ya robo fainali, ni kusaka ushindi ambao utaendelea kuwaweka kwenye mazingira salama.
Kwa upande wa wenyeji wao AS Monaco, watalazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuendelea, ili kufanikisha mpango wa safari yao ya kuelekea hatua ya robo fainali.
Michuano hiyo inaendelea tena hii leo kwa michezo ya 16 bora mkondo wa pili kuchezwa, ambapo mabingwa wa soka nchini Italia Juventus watakua nyumbani mjini Turin wakiwakabili mabingwa wenzao kutoka nchini Ureno FC Porto.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Juventus walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.
Mchezo mwingine utashuhudia mabingwa wa soka nchini England Leicester City wakipapatuana na Sevilla CF kutoka Hispania kwenye uwanja wa King Power.
Mchezo wa mkondo wa kwanza Sevilla CF, walipata ushindi wa mabao mawili kwa moja.