Mshambuliaji Romelu Menama Lukaku ameuambia uongozi wa klabu ya Everton hatosaini mkataba mpya kama walivyokua wakitarajia siku kadhaa zilizopita.

Lukaku amechukua maamuzi ya kuuambia wazi uongozi wa klabu hiyo ya Goodison Park, huku akielewa huenda akauzwa mwishoni mwa msimu huu.

Uongozi wa Everton tayari ulikua umeshaanza mkakati wa mazungumzo na mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji na ulijiandaa kumlipa mshahara wa Pauni 130,000 kwa juma.

Wakala wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, Mino Raiola, aliwahi kuwathibitishia waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa mchezaji wake kusaini mkataba mpya, kwa kusema kulikua na asilimi 99 ya jambo hilo kukamilishwa.

Kwa mantiki hiyo, Lukaku huenda akatimiza malengo ya kusaka changamoto mpya ya soka lake, baada ya kuwa na mazingira mazuri tangu aliposajiliwa moja kwa moja na klabu ya Everton mwaka 2014 akitokea Chelsea.

Kabla ya kusajiliwa moja kwa moja, Lukaku alipelekwa kwa mkopo huko Goodison Park msimu wa 2013/14 na msimu mmoja nyuma alicheza kwa mkopo katika klabu ya West Bromwich Albion.

Mkataba wa sasa wa Lukaku unatarajiwa kufikia kikomo mwaka 2019.

Dogo Wa Dodoma Akabidhiwa Jezi Ya Ajibu
Yusuf Manji Kupanda Tena Kizimbani