Washambuliaji tegemeo wa Yanga, Mrundi Amisi Joselyn Tambwe na Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma hawatasafiri na timu kwenda Zambia kwa mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco.
Tambwe hakucheza kabisa mchezo wa kwanza dhidi ya Zanaco Jumamosi ya Machi 11, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Ngoma alijitonesha goti katika mchezo huo baada ya kurejea kufuatia kuwa nje tangu Janauri.
Katibu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema pamoja na wawili hao ambao ni majeruhi, pia klabu itawakosa kipa Beno Kakolanya, beki Pato Ngonyani, kiungo Yussuf Mhilu na washambuliaji wengine wawili, wote wazawa, Malimi Busungu na Matheo Anthony ambao pia ni wagonjwa.
Mkwasa amesema wachezaji 20 ndiyo watasafari na timu hii leo kwa ndege ya Shirika la Kenya kwenda Lusaka kwa ajili ya mchezo huo wa Jumamosi, na kwa bahati mbaya hakutakuwa na mshambuliaji halisi hata mmoja.
Wachezaji wanaoatarajiwa kusafiri hii leo ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki ni Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Hassan Kessy, Juma Abdul, Vincent Bossou, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Justine Zulu, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Obrey Chirwa na Emanuel Martin.
Yanga inahitaji ushindi ili kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.