Mshambuliaji wa klabu ya Nice ya Ufaransa, Mario Balotelli amemkalipia mwandishi wa habari nchini humo baada ya kuulizwa kuhusu klabu yake ya zamani ya Liverpool.
Mwandishi wa RMC alimuhoji Balotelli kuhusu maisha ya soka la nchini Ufaransa tangu aliposajiliwa na klabu ya Nice mwanzoni mwa msimu huu, lakini alijikuta akimuuliza ni kitu gani anachokikosa tangu alipoondoka Liverpool.
Balotelli alimjibu mwandishi huyo kuwa hapendi kusikia swali ama taarifa zozote kuhusu Liverpool na kwamba kama alikuwa anataka kujua mambo mengine ni bora angemuuliza moja kwa moja na sio kupitia klabu hiyo ya England.
“Tafadhali usizungumzie kabisa kuhusu Liverpool hapa,” alisema. “Sipendi kuwa sehemu fulani halafu nikaulizwa swali la mahala ambapo niliwahi kupita na kuondoka. Suala hilo katika maisha yangu huwa silipi nafasi kabisa na wakati mwingine hunikasirisha. Ni sawa na mtu akakuuliza kuhusu maisha yako ya utotoni, kuna mambo hutopenda kuyazungumza kabisa,” aliongeza.
Alisema kuwa yeye ni mtu mzima na kwamba anajua anachokifanya hivyo kumtaka mwandishi kubaki kwenye mstari wa maswali yanayohusu Nice na sio Liverpool.
Balotelli aliondoka Liverpool mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuthibitishiwa na meneja wa klabu hiyo Jurgen Klopp, hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha wekundu hao wa Anfield.a