Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, wapo kwenye mikakati ya kumng’oa Mauricio Pochettino katika himaya ya White Hart Lane yalipo makao makuu ya klabu ya Tottenham Hotspur.
Gazeti la The Daily Mirror limechapisha habari kumuhusu meneja huyo raia wa Argentina, kwa kudai huenda akawa mbadala wa Unai Emery ambaye kwa sasa amekalia kuti kavu huko jijini Paris.
Emery ameingia shakani kutokana na kushindwa kuzuia kichapo cha mabao sita kwa moja walichokipokea kutoka kwa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Jambo lingine ambalo linamuweka shakani meneja huyo kutoka nchini Hispania, ni mwenendo wa ushindani katika ligi ya nchini Ufaransa ambapo PSG wapo kwenye hatari ya kupoteza ubingwa.
Kwa sasa klabu hiyo ya jijini Paris inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya Ufaransa, kwa tofauti na point tatu dhidi ya AS Monaco wenye point 68.
Uongozi wa PSG unaamini suluhiso la changamoto zinazowakabili msimu huu ni meneja wa Spurs Mauricio Pochettino, na tayari rais wa klabu hiyo Nasser Al-Khelaifi ameanza mipango ya kuhakikisha anamng’oa jijini London.
Endapo PSG watashindwa kumpata Pochettino, taarifa zinaeleza kuwa, huenda wakamgeukia meneja wa Arsenal Arsene Wenger anaemaliza muda wake wa mkataba.