Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wametakiwa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wanaowasimamia na kujali maslahi yao ili kuleta mageuzi makubwa ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Hayo yamesemwa mapema hii na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru wakati wa semina ya siku moja ya kuwakumbusha viongozi hao majukumu yao ya kila siku.
“Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, msilalamike kuhusu changamoto zinazowakabili, jambo mnalopaswa kufanya ni kutatua changamoto kwa manufaa ya hospitali ya Muhimbili,” amesema Prof. Museru.
Aidha, Profesa Museru amewaagiza wakuu wa Idara, wakuu wa Vitengo na Wakurugenzi kuhakikisha MNH inatoa huduma bora kwa kuzingatia wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kujenga miundombinu ya kisasa ya kutoa tiba kwa wagonjwa.
Kwa Upande wake, Mwakilishi Kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Magreth Mhando amesema MNH inatakiwa kuzingatia vipaumbele vya taifa katika Sekta ya Afya ambavyo ni kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto ili kupunguza vifo katika kundi hilo.
Hata hivyo, Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Makwaia Makani amewataka wakuu wa idara na vitengo kusimamia kwa makini utendaji kazi wa wafanyakazi wanaowasimamia kwa lengo la kuimarisha utoaji bora wa huduma kwa wagonjwa.