Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam mara mbili katika kesi zinazomkabili.
Katika kesi ya kwanza, askofu huyo anakabiliwa na shtaka la kushindwa kuhifadhi silaha, kesi ambayo alipata nafasi ya kujitetea mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Katika utetezi wake, Gwajima ambaye alikiri kukutwa na risasi 17 kwenye begi lake Machi 27 mwaka 2015, alidai kuwa aliacha bunduki nyumbani kwake ili endapo mtu ataiiba asikute ikiwa na risasi huku akisisitiza kuwa amiliki silaha hizo kihalali.
Alieleza kuwa alijisalimisha katika ofisi ya Ofisa wa Upelelezi (ZCO) Kanda Maalum ya Dar es Salaam baada ya kuona kwenye mitandao ya kijamii kuwa anatafutwa wakati akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kwenye mkutano wa Maaskofu.
Aliiambia Mahakama hiyo kuwa akiwa katika ofisi hiyo aliwakuta watu 30, lakini hakupata nafasi ya kujieleza kwani alijikuta akipoteza fahamu baada ya kuvuta vumbi la chaki kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa akikung’uta gazeti.
“Alikuwepo mtu mmoja ameshika gazeti analikung’uta, nikasikia harufu ya chaki ikinipalia nikapiga kelele, ‘kuna kitu kinanipalia’ kisha nikaanguka chini nikapoteza fahamu,” alisema.
Gwajima alidai kuwa baada ya hapo alijikuta katika hospitali ya Oysterbay Polisi jijini Dar es Salaam na kwamba alimuona askari mmoja akitaka kumchoma sindano. Hata hivyo, alidai kuwa baada ya hapo alijikuta yuko katika hosptali ya TMJ akipatiwa matibabu.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 10, ambapo inatarajiwa kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo. Gwajima anatetewa na wakili Peter Kibatala.
Katika kesi nyingine iliyosomwa mahakamani hapo dhidi ya Gwajima, ni shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kadinali Pengo, Machi 16 na 25 mwaka 2015 katika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 12 na 13 mwaka huu, huku Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha alidai kuwa mwenendo wa kesi hiyo hauna historia nzuri kwani upande wa mashtaka umeshaita shahidi mmoja tu.
Hakimu alitahadharisha kuwa endapo mambo hayataenda ipasavyo kwa upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi wanaotakiwa, Mahakama itafanya kile inachokiona ni sahihi.