Aliyekua mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametuma salamu kwa timu alizokuwa akipambana nazo wakati akiwa anakinoa kikosi hicho cha Jangwani, baada ya kumwaga wino wa kuanza kuiona Singida United.
Pluijm ambaye aliondolewa Yanga kupitia barua iliyotaja kuyumba kiuchumi kama sehemu ya sababu za kushindwa kuendelea kummudu, amesema kuwa amefurahi kupata timu ya kuifundisha hapa nchini hivyo atatumia fursa hiyo kuonesha uwezo wake halisi hususan katika msimu ujao wa Ligi.
Salam za kocha huyo hazikuiweka kando timu ya Yanga, ambapo amedai kuwa ni muda wa kuzinyoosha timu zote ikiwemo timu hiyo aliyofanya nayo kazi akishika nafasi mbili tofauti, baada ya kumpisha Mzimbia, George Lwandamina na kuwa bosi wa benchi la ufundi.
“Kiukweli namshukuru Mungu kwa sababu zimekuja ofa nyingi lakini bado nina mapenzi na soka la Tanzania, hivyo kuwepo kwangu hapa katika timu hii kuna maana kubwa sana,” alisema.
“Kikubwa nataka kuwaaminisha watu ukweli halisi kuhusu uwezo wa kazi yangu, naomba Mungu anisaidie katika kila kitu ili kufikia lengo hilo, kwani nahitaji kufanya vizuri nikiwa na timu yangu mpya kwenye ligi ya msimu ujao, bila ya kuangalia timu ipi nitakutana nayo,” alisema Pluijm.
Timu ya Singida United ina matumaini makubwa na kocha huyo Mholanzi na wanaamini atawaweka katika nafasi nzuri zaidi sio tu katika Ligi ya Tanzania bali hata kuwapa nafasi nje ya mipaka ya nchi.