Kiungo wa klabu ya Chelsea, Eden Hazard ameondolewea kwenye kikosi cha timu ya taifa lake la Ubelgiji ambacho kwa sasa kipo kambini kikijiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Ugiriki utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez amethibitisha kumuondoa kiungo huyo baada ya kubainika hatoweza kupona kwa haraka jeraha la kiazi cha mguu, ambalo alilipata akiwa kwenye mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa ligi ya England uliyowakutanisha na Stoke City mwishoni mwa juma lililopita.
Martinez amesema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, alifanyiwa vipimo na jopo la madaktari wa kikosi cha Ubelgiji, na amebainika kuwa na majeraha.
Katika hatua nyingine kiungo wa Man Utd Marouane Fellaini pamoja na beki wa kulia wa Paris Saint-Germain Thomas Meunier, jana walikosa mazoezi ya kikosi cha Ubelgiji.
Fellaini aliamuriwa kupumzika baada ya kufanya kazi kubwa wakati wa mchezo wa ligi ya England dhidi ya Middlebrough siku ya Jumapili. Kwa upande mwingine, Meunier akibainika kuwa na majeraha ya kifundo cha mguu ambayo yatamuweka nje kwa siku kadhaa.
Timu ya taifa ya Ubelgiji inaongoza kundi H, baada ya kushinda michezo minne ya kundi hilo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018, na wanakwenda kupambana na Ugiriki ambayo haijapoteza mchezo.