Klabu ya Manchester City imefunguliwa mashtaka na chama cha soka nchini England (FA), kufuatia utovu wa nidhamu ulionyeshwa na wachezaji wa klabu hiyo, wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Liverpool uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.
Taarifa iliyotolewa na FA inaelekeza kuwa, wachezaji wa Man City walionyesha utovu wa nidhamu dakika ya 50, kwa kumzonga mwamuzi Michael Oliver, na kupinga adhabu ya mkwaju wa penati ambayo iliipa uongozi Liverpool kwenye mchezo huo uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Mwamuzi Oliver aliamuru mkwaju huo upigwe kwenye lango la Man City, kufuatia beki wa pembeni Gael Clichy kumfanyia madhabi kiungo mshambuliaji wa Liverpool Roberto Firmino. Aliyekua mshambuliaji wa Man City James Milner, alikwamisha mkwaju huo wa penati.
Kwa kitendo cha kumzonga mwamuzi, kiungo David Silva alionyeshwa kadi ya njano.
Hata hivyo Man City walisawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wao kutoka nchini Argentina Sergio Kun Aguero.
FA wametoa muda hadi saa kumi na mbili jioni siku ya Alhamisi, kwa kuitaka klabu ya Man City kukubali ama kukataa mashataka ya utovu wa nidhamu yaliyofunguliwa dhidi yao.