Mazungumzo na kusaini mkataba mpya yanayowahusu wachezaji wawili wa Arsenal Mesut Ozil na Alexis Sanchez yamesitishwa kwa muda hadi mwishoni mwa msimu huu.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amethibitisha kusitishwa kwa mazungumzo hayo, ambayo yalitarajiwa kutoa mustakabali na wachezaji hao wawili kabla ya msimu huu wa 2016/17 kufikia kikomo mwezi Mei.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha beIN Sports, Wenger alisema maamuzi ya kusitishwa kwa mazungumzo hayo yamefanywa kwa lengo la kutoa nafasi kwa mambo mengine kuchuku mkondo wake klabuni hapo.
Mshambuliaji kutoka Chile Sanchez, ambaye kwa sasa anaongoza kwa kupachika mabao 18 miongoni mwa wachezaji wa Arsenal kwa msimu huu pamoja na kiungo kutoka Ujerumani Ozil, wote kwa pamoja wamesaliwa na muda wa mwaka moja katika mikataba yao.
“Kwa sasa tumeamua kusitisha mazungumzo ya kusaini mikataba ya wachezaji hawa wawili, tumeona jambo hili liendelezwe mwishoni mwa msimu huu ili kupisha shughuli nyingine za klabu kuendelea,” Alisema Wenger.
“Tumejipanga kwa mambo mengi ili kutimiza malengo yetu katika kipindi hiki cha michezo ya ligi na michuano mingine inayoendelea, tunaamini hakuna litakaloshindikana katika mazungumzo ambayo tutayafanya mwishoni mwa msimu huu.” Aliongeza Wenger
Arsenal imekua na wakati mgumu wa kuwashawishi wawili hao kusaini mkataba mpya, baada ya kuwa katika hali ya sintofahamu ya ushindani wa kusaka mataji kwa msimu huu, kutokana na mambo kwenda mrama.
Kipigo cha jumla cha mabao 10-2 kilichotolewa na mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kinatajwa kuvuruga mazungumzo yaliyokua yanawahusu wachezaji hao wawili ambao huenda wakaondoka mwishoni mwa msimu huu.