Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdul-Aziz Abood, ametangaza kuwa hatagombea tena nafasi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).
Akizungumza hivi karibuni katika moja ya vikao vya ndani vya chama mjini humo, Abood alisema kuwa amekitumikia chama kwa muda mrefu, hivyo anaona hana budi kuwaachia nafasi watu wengine huku akisisitiza kuwa ataendelea kuwania nafasi ya ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Aidha, Mbunge huyo alitoa wito kwa wanachama wote wa CCM kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za mwenyekiti wa chama hicho, Dkt. John Magufuli zinazolenga katika kukiimarisha zaidi.
Mbunge huyo ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu mjini humo alisisitiza kuwa mabadiliko yanayofanywa ndani ya CCM, yataleta mageuzi yatakayokiimarisha zaidi.
Moja kati ya mabadiliko yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa CCM taifa kwenye mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho hivi karibuni mjini Dodoma, ni pamoja na kuwaondoa makatibu wa ngazi ya wilaya kuhudhuria mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho.