Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na operesheni katika maeneo mbalimbali mkoani humo na kufanikiwa kukamata wafanyabiashara wakiwa na Pombe Kali zilizopigwa marufuku pamoja na watumiaji wa pombe hizo.
Polisi Mbeya wamefanya msako huo kufuatia mapambano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa Pombe kali ( Viroba) zilizopigwa marufuku.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishina wa Polisi Dhamira A. Kidavashari amesema kuwa katika Operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa 09 ambao pia ni wafanyabiashara walikamatwa wakiwa na Pombe hizo zilizopigwa marufuku katika msako uliofanyika katika maeneo ya Uyole, Kabwe, Sae, Mwanjelwa Jijini Mbeya, Kyela kati, Kalumbulu – Kyela, Ngyekye – Kyela, Rujewa – Mbarali na Kibaoni – Chunya, mkoani Mbeya.
Pia, jumla ya katoni 105 za Pombe kali aina ya Konyagi (viroba original) zilikamatwa na paketi 106 za Konyagi (viroba original). Pia zilikamatwa pombe kali zilizopigwa marufuku aina mbalimbali ambazo ni value auter katoni 14, viroba aina ya “high life” paketi 180, Fiesta paketi 450, (viroba) paketi 340 aina ya ridder, gun paketi 165 na chupa za ridder 60 na paketi 9,840 aina ya Shujaa.
Jeshi hilo la Polisi limeendelea na msako mkali dhidi ya pombe hizo zilizopigwa mafuruku ambapo hadi kufikia tarehe Machi, 24, 2017 jumla ya Katoni 11,598 na Paketi 11,987 za Pombe kali zilizopigwa marufuku na Serikali zikiwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) zimekamatwa.
Aidha, Kamanda Kidavashari ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu na mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na biashara ya Pombe kali zilizopigwa marufuku pamoja na dawa za kulevya ili wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Pia Kamanda huyo amewataka wananchi kufanya kazi na kuacha kujihusisha na biashara ya Pombe Kali zilizopigwa marufuku pamoja na uhalifu kwa ujumla kwani Jeshi la Polisi halitavumilia aina yoyote ya uhalifu.