Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli inautashi wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezani na biashara nchini kwa kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja nchini.
Majaliwa amesema hayo Machi 23,2017 wakati akifungua kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lilifanyika katika Hotel ya Labourdonnaise mjini Port Louis nchini Mauritius.
Kongamano hilo liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Majaliwa amesema Tanzania ina uchumi imara unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya biashara bila ya kuingiliwa na Serikali, hivyo sekta binafsi imepewa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli nawakaribisha kwa mikono miwili kuja na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii na kutembelea vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake na kwa wafanyabiashara Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.
Amesema kuwa TIC na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kwa pamoja vimeweka taratibu ambazo zinamwezesha mwekezaji kupata mahitaji yake muhimu ya kuwekeza katika kituo kimoja (One stop Centre).
Majaliwa amesema kuwa Tanzania inatarajia wawekezaji pia kutoka Mauritius kwani kwa sasa wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wanatoka katika mataifa mbalimbali kama Marekani, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Autsralia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
“Ujio wa wawekezaji hawa haukuwa wa bahati bali ni kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali pamoja na suala zima la soko kubwa la bidhaa zao na huduma. Soko hili linalozidi watu milioni 300 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika linatoa uhakika wa soko kubwa kwa mwekezaji yeyote anayekuja Tanzania kuwekeza,”.
Majaliwa pia ameeleza kuwa kuwekeza nchini Tanzania kunampa fursa mwekezaji kupata fursa maalumu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na soko la nchi ambazo hazipakani na bahari.