Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo amezitaka taasisi za Serikali na binafsi za uchapishaji kuendelea kujisajili katika Ofisi hiyo na kuepuka usumbufu wa kubainika kwenye msako.
Ameyasema hayo mapema hii leo mara baada ya kutoridhishwa na kasi ya kampuni za uchapishaji zilizojitokeza kujisajili tangu wito huo utolewe Februari 13, mwaka huu, ambapo ni kampuni 24 tu tayari zimejitokeza.
Amesema kuwa amesikitishwa na mwitikio mdogo wa usajili wa kampuni na taasisi za uchapishaji, hivyo ameamua kutumia fursa ya kuwakumbusha watimize wajibu wao kisheria.
“Inawezekana katika mkutano wangu sikueleweka vizuri lakini usajili unahusu kampuni binafsi na Serikali kwa lengo la kutambua shughuli zao na kuepuka kujificha,” amesema Chibogoyo.
Aidha, Chibogoy ameziagia taasisi hizo kwenda kujisajili kabla ya kumalizika kwa muda wa siku tano zilizobakia, kwani baada ya hapo Serikali itaanza kuchukua hatua kali kwa taasisi zote ambazo zinajihusha na uchapishaji huku hazijasajiliwa.
Vile vile amesema kuwa Wachapishaji halali watakaojiorodhesha watakaribishwa na kupewa fursa ya kutoa mawazo ya kuiweka nchi mahali salama kupitia nyaraka.
Hata hivyo, hatua hiyo imechukuliwa ili kupiga vita wachapishaji wa nyaraka bandia kwa kuwasaka nyumba kwa nyumba, iwapo watashindwa kujitokeza na kujisajili kwa hiari.