Timu ya taifa ya Madagascar imejihakikishia nafasi ya kucheza michezo ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2007, baada ya kuifunga Sao Tome and Principe mabao 3-2.
Ushindi huo uliopatikana katika ardhi wa mji wa Antananarivo ulitanguliwa na ule wa bao moja kwa sifuri walioupata siku tano zilizopita mjini São Tomé. Hivyo, Madagascar wanasonga mbele kwa jumla ya mabao manne kwa mawili.
Masdagascar wanaingia kwenye kundi A ambalo lina timu za Senegal, Equatorial Guinea na Sudan kwa ajili ya kuwania kufuzu fainali za Afrika za 2019, na mchezo wao wa kwanza utacheza mjini Khartoum mwezi Juni.
Madagascar iliwahi kupata nafasi kama hiyo mwaka 2010, katika harakati za kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia kwa kuifunga Comoro jumla ya mabao kumi kwa mawili.
Mchezo wa kwanza Madagascar walipata ushindi wa mabao sita kwa mbili na mchezo wa mkondo wa pili waliishinda Comoro mabao manne kwa sifuri.