Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele leo Machi 27, 2017 amekabidhi ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Faru John, ambapo amesema kuwa tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru huyo kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa na kubaini kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya Faru mweusi ambaye ni dume.
Prof. Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa Faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.” amesema.
Ameongeza kuwa sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozi kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake.
Aidha, kuna mapungufu yaliyobainika kutokana na uchunguzi huo ambayo yametajwa kuwa ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John, kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Prof. Manyele ameendelea kuyataja mapungufu mengine kuwa ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.
Prof. Manyele amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.
Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa mengine.
Mwisho Prof. Manyele ameshauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).