Baada ya Serikali kupiga marufuku uuzaji na unywaji wa pombe kali aina ya viroba, wanywaji wa pombe hizo Mkoani  Dodoma wamebuni mbinu mpya ya kununua pombe hiyo iliyopigwa marufuku huku watumiaji hao wakiipa pombe hiyo jina la maziwa mgando.
Aidha, uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mtanzania kwa siku kadhaa mkoani Dodoma, umeonyesha jinsi pombe hiyo inavyouzwa kwa shilingi 1,000 baada ya kujazwa kwenye chupa kubwa za konyagi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa pombe hiyo amesema kuwa biashara hiyo imekuwa ni ngumu na wao wanahitaji kupata fedha, hivyo wameamua kuja na mbinu mpya ya kuuza viroba hivyo itakayo wawezesha kuendelea kujipatia kipato.
“Tutafanyaje ndugu yangu, maisha magumu, tumeweka viroba katika chupa kubwa za konyagi na tunawapimia kwa kutumia kakikombe kadogo kama ka kahawa kwa shilingi 1,000,” amesema mfanyabiashara huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Amesema kuwa hawezi kuacha kufanya biashara hiyo kwani hapo mjini Dodoma  hasa maeneo ya Stendi ya mabasi wateja wao wakubwa ni wasafiri na makondakta ambao huwapatia fedha za kutosha, lakini kutokana na  hali ilivyo kwa sasa anauza kwa watu anaowafahamu tu na si vingine kwa hofu ya kukamatwa.
Hata hivyo, mmoja wa wanunuzi wa viroba hivyo, amesema kuwa baada ya Serikali kupiga marufuku uuzwaji wa viroba hivyo, wameamua kubadili mwelekeo wa kununua bidhaa hiyo ili kukwepa mkono wa Serikali.

Magazeti ya Tanzania leo Machi 28, 2017
Young Africans Kuikacha Dar es salaam