Majogoo wa jiji Liverpool wana matumaini makubwa ya kumuuza moja kwa moja beki wao kutoka nchini Ufaransa Mamadou Sakho ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Crystal Palace kwa mkopo.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 27, alisajiliwa na Liverpool kwa kiasi cha Pauni milioni 18 akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, na thamani yake kwa sasa inakadirisha kufikia kiasi hicho ambacho hakitaipa hasara The Reds.
Sakho bado ana mkataba na klabu ya Liverpool hadi mwaka 2020, jambo ambalo linaendelea kuipa jeuri klabu hiyo ya Anfield, kwa kuamini thamani yake haitoshuka.
Crystal Palace imeshawasilisha ombi la kutaka kumsajili moja kwa moja beki huyo, huku Southampton wakiwa na lengo kama hilo, hivyo kuna dalili za biashara ya mchezaji huyo ikafanyika mwishoni mwa msimu huu.
Klabu nyingine inayotajwa kuwa kwenye mpango wa kumsajili Sakho ni SSC Napoli ya Italia.
Sakho alishindwa kumshawishi meneja wa Liverpool Jurgen Klopp ili acheze katika kikosi cha kwanza, na badala yake alijikuta akikaa benchi kwa zaidi ya miezi sita kabla ya kuuzwa kwa mkopo mwezi Januari.