Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mparange na mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Ikwiriri Kaskazini ,wilayani Rufiji Mkoani Pwani, Michael Lukanda,ameuawa kwa kupigwa risasi kichwani na watu wasiojulikana.
Watu hao wanadaiwa kuwa ni wawili waliotumia usafiri wa pikipiki ambapo mmoja alimpiga risasi marehemu mlangoni akiwa anataka kuingia nyumbani kwake kisha kutokomea kusikojulikana.
Tukio hilo limefuatia baada ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mparange kijijini hapo, Bakari Mpanawe kunusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya tumboni na mkononi march 19 mwaka huu.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amekiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia march 29.
Amesema kuwa tukio hilo ni la tano kutokea ndani ya mwezi huu, likihusisha uhalifu wa kutumia silaha za moto .
“Tunaendelea kuwasaka watu waliohusika na kufanya matukio haya yote ndani ya mwezi huu ili tuweze kuwachukulia hatua za kisheria,” amesema Kamanda Lyanga.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Kibiti, Zena Mgaya amesema hali ya usalama sio shwari katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kibiti na Rufiji kijumla.
Zena amesema kuwa, matukio ya aina hiyo yanawasababishia kuishi kwa hofu pasipo na amani na wanachama wa CCM kuhofia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo za chama na Serikali za vijiji na vitongoji.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Dimani, Ramadhani Manyema amesema kuwa kuna wenyeviti wa vitongoji na vijiji vinne wamekimbia miji yao wakihofia maisha yao .
Hata hivyo, Manyema amesema kuwa kukimbia maeneo yao ya kazi kumetokana na kutokea matukio ya hivi karibuni ambapo Mwenyekiti wa kijiji cha Nyambonda pamoja na Wenyeviti wa vitongoji viwili na Mtendaji wa Kijiji hicho kupigwa risasi, ameyataja maeneo mengine ambayo yamekuwa matukio kama hayo ni Jaribu Mpaka ambako OC CID na Mgambo wa Maliasili walipigwa risasi na kufariki.