Mshambuliaji Alexis Sanchez amesema atafanya maamuzi sahihi kuhusu mustakabali wa kuendelea kuitumikia Arsenal ama la, kupitia mazungumzo ya mkataba mpya, ambayo yataendelea mwishoni mwa msimu huu.
Sanchez amefunguka kuhusu mustakabali wake, siku moja baada ya uongozi wa Arsenal kuhusishwa na taarifa za kutaka kumuweka sokoni kwa dau la Pauni milioni 50, endapo utashindwa kufanikisha mpango wa kumsainisha mkataba mpya.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Chile, amesema anapenda maisha ya jijini London na tangu alipotua jijini humo amekua na mahusiano mazuri na kila mtu wake wa karibu, hivyo halitokau jambo la busara kuondoka ili hali bado anaunda mji huo mashuhuri nchini England.
Hata hivyo Sanchez amesema dhamira yake ni kutaka kucheza soka katika klabu yenye kikosi bora na ushindani dhidi ya timu yoyote duniani, hivyo anaamini suala hilo litakua na mashiko kwenye mazungumzo yake na viongozi wa The Gunners mwishoni mwa msimu huu.
Lakini pamoja na msisitizo huo, bado mashabiki wa soka duniani wanaamini huenda Sanchez akawa amewatega viongozi wa Arsenal kwa kuwashinikiza kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango vya hali ya juu ili kutengeneza kikosi imara kwa msimu ujao wa ligi.
Wengine wanaamini kauli ya Sanchez huenda ikawa inaitikia wito wa matamanio ya meneja wa Chelsea Antonio Conte, ambaye ameonyesha kuwa tayari kutuma ofa huko kaskazini mwa jijini London, ili kufanikisha dhamira yake ya kumsajili kwenye kikosi cha The Blues ambacho kina sifa alizozitaja.
Klabu nyingine zinazohusishwa na mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji huyo ni Juventus, PSG, Bayern Munich na Man Utd.
Sanchez ni miongoni mwa wachezaji wa Arsenal ambao wamesaliwa na mkataba wa miezi 18, huku wengine ni Mesut Ozil na Aaron Ramsey.