Vita ya mipango ya usajili imeibuka kati ya meneja wa Chelsea Antonio Conte dhidi ya mkurugenzi wa ufundi Michael Emenalo kuhusu usajili wa mshambuliaji ambaye ataziba nafasi ya Diego Costa.

Wawili hao wamepishana katika dhamira ya mapendekezo ya usajili wa mshambuliaji, na tayari kuna majina ya Romelu Lukaku wa Everton na  Alvaro Morata wa Real Madrid ambao mmoja wao atastahili kusajiliwa mwishoni mwa msimu huu.

Antonio Conte amempendekeza Morata na mkurugenzi wa ufundi Emenalo anaamini Lukaku atafaa kuziba nafasi ya Costa ambaye huenda akaondoka mwishoni mwa msimu huu.

Conte anaamini uwezo wa Morata utakidhi mipango ya ushambuliaji ya kikosi chake msimu ujao wa ligi, kutokana na kumfahamu vilivyo mshambuliaji huyo, ambaye aliwahi kuitumikia Juventus ya Italia kabla ya kurejea nyumbani mjini Madrid mwanzoni mwa msimu huu.

Meneja huyo kutoka nchini Italia anahisi uzoefu na umahiri wa mshambuliaji huyo wa kispaniola una kiwango cha hali ya juu kwa sasa, licha ya kutotumika mara kwa mara katika kikosi cha Real Madrid.

Kwa upande wa Emanalo anatetea usajili wa Lukaku kutokana na mshambuliaji huyo kuyafahamu vyema mazingira ya klabu ya Chelsea ambayo ilimsajili mwaka 2011 akitokea Anderlecht, kabla ya kumtoa mara mbili kwa mkopo na kisha kumuuza moja kwa moja huko Goodison Park.

Emenalo amewasilisha utetezi wake mbele ya viongozi wa juu wa Chelsea akidai kuwa, Lukaku ana uzoefu mkubwa katika soka la England tofauti na Morata ambaye atalazimika kuchukua muda wa miezi hadi mwaka ili azoee  mikiki mikiki ya ligi hiyo pendwa duniani.

Tayari Lukaku ameshakataa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Everton, na huenda mwishoni mwa msimu huu akaingizwa sokoni endapo uongozi wa The Toffees hautokubali kuingia hasara ya kumuachia aondoke kama mchezaji huru.

Wanne Kuikosa West Bromwich Albion
Alexis Sanchez Aigawa Arsenal