Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi, Willbrod Slaa amesema anajitathmini kwa kile kilichomfanya aondoke hapa nchini na familia yake kama hakipo aweze kurejea nyumbani.
Dkt. Slaa aliamua kuweka pembeni masuala ya siasa baada ya kutofautiana na chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea wa Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Amesema kuwa kwa sasa amemaliza masomo yake na baada ya kutafakari na kujitathmini atarejea nyumbani muda wowote.
“Ni kweli nimemaliza masomo yangu, bado napima mazingira yaliyonifanya niondoke na familia yangu, baada ya hapo nitaangalia uwezekano wa kurejea nyumbani,”amesema Dkt. Slaa.
Aidha, kuhusu mwenendo mzima wa Serikali ya awamu ya Tano, amesema kuwa hakuna nchi hata moja ulimwenguni ambayo Rais wake atakubarika kwa asilimia mia moja, hivyo Rais Magufuli ameonyesha msimamo wa kusimamia kile anachokiamini
Hata hivyo, ameongeza kuwa kama wapinzani hawatakuja na ajenda makini na mkakati unaoweza kuwasaidia wananchi hapo walipo, basi upinzani unaweza kufutika mwaka 2020.