Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejikuta katika wakati mgumu baada ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Thomas Kashillilah kudai kuwa hawakutimiza vigezo vya wagombea wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kikiwemo kigezo cha uwiano wa jinsia.
Chadema ambayo ina nafasi mbili kwenye EALA, iliwasilisha majina ya wagombea wawili ambao ni Lawrence Masha na Ezekia Wenje.
Akizungumzia vigezo vingine, Dk. Kashillilah alisema kuwa Chadema haikuwasilisha fomu ya matokeo ya kura za kuwapitisha na kukosekana kwa fomu ya maombi ya wagombea na orodha ya waombaji.
Dk. Kashillilah ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo amesema kuwa ameviandikia barua vyama vya upinzani kikiwemo chama cha CUF kuvitaka kufanya marekebisho na kuyawasilisha leo kabla ya saa saba mchana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameeleza kushangazwa na kizingiti cha vigezo hivyo na muda wa saa 24 uliotolewa huku akisisitiza kuwa hawatabadili wagombea waliowawasilisha.
Mbowe amedai kuwa kinachofanyika ni hila za CCM kutaka kuingilia upande wa maamuzi ya upinzani kwani walishakaa kwenye vikao vya kanuni na kujadiliana lakini hoja hiyo imeibuka jana. Alisema mabadiliko hayo hayatekelezeki kwa saa 24 kwani yanapaswa kufanywa na vikao kadhaa vya chama kuwapata wagombea wengine.
“Kamati Kuu imeshakaa na imetuchagulia hao tuliowapelekea. Kiukweli sharti hili halitekelezeki na hatutalitekeleza,” alisema Mbowe. “Tutatafuta haki yetu ndani ya Bunge, ikishindikana tutaenda kuitafuta mahakamani,” Mbowe anakaririwa na Mwananchi.
Kwa upande wa CUF, bundi la mgogoro kati ya upande unaomuunga mkono mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na kundi linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad limeendelea kuibua vurugu hadi kwenye uchaguzi huo.
Pande zote mbili zimewasilisha wagombea huku ofisi ya Bunge ikiwasiliana na pande zote kwa wakati mmoja. Upande wa Maalim Seif wamewasilisha jina moja la mgombea huku upande wa Lipumba ukiwasilisha majina matatu.
Kila upande umejinasibu kuwa ndio wenye haki ya kutoa wagombea.