Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha athari kubwa katika maeneo ya Chalinze, ambapo mpaka sasa hakuna mawasiliano ya barabara kutoka Kata ya Vigwaza na Mwavi Jimbo la Chalinze.
Aidha, hali hiyo imesababisha wakazi wa maeneo hayo kuvushwa kwa msaada wa kubebwa mgongoni na shingoni kwa gharama ya sh.3,000 na 2,000 na pikipiki kupitishwa kwa sh.5,000 huku magari yakishindwa kupita kabisa.
Mmmoja wa wakazi wa maeneo yaliyoathirika, Zinabu Zuberi aliyekuwa akivushwa kuelekea upande wa pili amesema kuwa wanaiomba Serikali kutoa huduma ya dharula ya mawasiliano kwani kwa sasa wanapata shida hasa kipindi hiki cha Mvua.
“Barabara ni mbovu kama mnavyojionea, haipitiki watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani ,tatizo hapa ni barabara imejengwa bila kuwekewa makaravati ndio maana imesombwa yote na maji,”amesema Zainabu.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa hali iliyopo kwa sasa hairidhishi na inampa wakati mgumu na wakazi wa maeneo hayo, hivyo ameahidi kuisimamia kero hiyo kwa kuifikisha Bungeni na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili lifanyiwe kazi.