Beki wa Wekundu Wa Msimbazi Simba Abdi Banda, anatarajia kuondoka nchini kesho Jumatano kwenda Afrika Kusini huku Kamati ya saa 72 ikiwa imemsimamisha kwa kosa la kumpiga ngumi nahodha wa Kagera Sugar George Kavila.
Kamati hiyo itakutana tena Alhamisi juma hili kujadili kwa kina juu ya kitendo alichokifanya Banda, wakati wa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, ambao walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.
Wakati kamati ya saa 72 ikitarajiwa kutangaza maamuzi dhidi ya Banda, tayari mchezaji huyo wa zamani wa Coastal Union amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya safari ya kuelekea Afrika kusini.
Akiwa nchini humo, Banda atafanya mazungumzo ya kusaini mkataba na moja ya timu za Afrika kusini, ingawa taarifa za awali zilisema angekwenda kufanya majaribio katika klabu ya Kaizer Chief mwezi ujao.
Banda ameiambia Dar24 kuwa, “Sitachukuwa muda mrefu halafu nitarejea maana sijui maamuzi yao yatakuwa vipi, ila siendi kwenye majaribio ni mazungumzo tu ambayo hayatachukuwa hata wiki.
“Ila nitakosa mechi hii ya Mbao na ijayo dhidi ya Toto African, nimewaaga viongozi wangu pia wanafahamu juu ya hii safari, haya ni maisha yangu kupitia soka hivyo natakiwa niangalie kote kote pale,” alisema Banda.
Banda anamaliza mkataba wake na Simba mwisho wa msimu huu na tayari alifanya mazungumzo na vigogo hao ambapo imebaki kusaini tu mkataba ambao ameushika mkononi akiwa anapitia baadhi ya vipengele.
Kuhusu hilo Banda alisema, “Simba ndiyo timu niliyoipa kipaumbele ila hadi sasa hatujamaliza, imetokea hii nafasi naenda kuwasikilizia mengine tutajuwa hapo baadaye.”