Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema mustakabali wake ndani ya klabu hiyo hauwaathiri wachezaji, lakini amekiri kipigo cha mabao matatu kwa sifuri kilichotolewa na Crystal Palace usiku wa kuamkia hii leo kilikuwa tatizo kubwa.
Wenger bado hajasaini mkataba mpya kufuatia mkataba wa sasa kutarajia kumalizika mwishoni mwa msimu huu, huku akiwa tayari ameandaliwa mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuwafundisha ‘Washika bunduki’ japo kuwa hajatangaza kama ataendelea au la.
Matokea ya jana usiku yameitupa Arsenal hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi huku ikibakisha michezo tisa pekee.
“Nimesimamia zaidi ya michezo 1,100 kwa Arsenal ila hatujazoea kupoteza michezo kama hivi. Tunapaswa kuchukua hatua haraka sana na sio kukubali.” Alisema Wenger.
Baadhi ya mashabiki waliosafiri na timu walimwambia Wenger anatakiwa kuondoka klabuni hapo kwakuwa hana jipya tena.
Mabao yaliyofungwa na Andros Townsend, Yohan Cabaye na Luka Milivojevic yamefanya kipigo hicho kuwa cha nne mfululizo kwa Arsenal na ni mara ya kwanza tangu Wenger aanze kufundisha miaka 21 iliyopita.
Hii inawafanya Arsenal kuwa kwenye hatari ya kushindwa kumaliza kwenye nafasi nne za juu na itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mfaransa huyo mwenye miaka 67.
“Naelewa mashabiki wetu hawana furaha, na sisi wote kwa ujumla hatuna furaha pia.
“Inasikitisha jinsi tulivyopoteza mchezo huu. Palace walikuwa na kasi, waliwafunga Chelsea siku zilizopita na wameonyesha wana uwezo wa kufanya vizuri.
“Tupo kwenye nafasi ngumu na matokeo ya mchezo huu hayakutusaidia,” alisema Wenger.