Baadhi ya Kampuni za simu hapa nchini zinazotoa huduma chini ya kiwango zimetozwa faini ya shilingi milioni 695 kwa kutokidhi vigezo vya huduma zao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, amesema kuwa Kampuni hizo zimetozwa faini hiyo kwa kwenda kinyume cha sheria na makubaliano.
Amesema kuwa tangu Mamlaka hiyo ijiwekee utaratibu wa kupima ubora wa kila robo ya mwaka, wamebaini ukiukwaji mkubwa wa utoaji wa huduma katika mikoa ya Mbeya, Dar es salaam na Iringa kuwa uko chini ya kiwango.
“Utoaji wa huduma zisizokidhi vigezo vya ubora una athari kubwa kwa watumiaji, hivyo kwa Mamlaka iliyopewa TCRA imezitoza faini Kampuni hizi,”amesema Kilaba.
Aidha, Kilaba amesema kuwa katika kudhibiti utoaji wa huduma katika Makapuni ya simu hapa nchini, kila robo ya mwaka TCRA imekuwa ikipima ubora wa huduma zitolewazo na kila Kampuni kulingana na sheria na taratibu za nchi zilizowekwa.
Hata hivyo, ameyataja makampuni yaliyopigwa faini kuwa ni pamoja na Airtel Tanzania Limited (sh milioni 55), Benson Informatics Limited-smart (sh milioni120), MIC Tanzania Limited-Tigo (sh milioni 120), Vodacom Tanzania Limited (sh. milion 115), Zanzibar Telecom Limited-Zantel (sh milioni140), Viattel Tanzania Limited-Halotel (sh milioni 50) na Tanzania Telecommunication-TTCL (sh milioni 95).