Kiungo Jack Wilshere ameingia kwenye mashaka ya kukosa sehemu ya msimu wa 2016/17 iliyosalia, kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Tottenham Hotspurs uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.
Kiungo huyo anaeitumikia klabu ya AFC Bournemouth kwa mkopo akitokea Arsenal, alipata maumivu wa mguu wake wa kushoto baada ya kuchezewa rafu na mshambuliaji wa Spurs Harry Kane.
Majibu ya vipimo vya X-Ray yaliyotolewa kwa awamu mbili, yanaonyesha mguu wa kiungo huyo umevunjika na huenda ukashindwa kuunga ndani ya siku zilizosalia kabla ya msimu huu kufikia kikomo mwezi ujao.
Bado taarifa rasmi hazijatolewa na meneja wa AFC Bournemouth Eddie Howe kama ataweza kumtumia kabla ya msimu huu kumalizika, lakini wasiwasi umetawala miongoni mwa watu wa benchi la ufundi kuhusu uhakika wa jambo hilo.
Wilshere mwenye umri wa miaka 25 aliwahi kukosa sehemu ya msimu wa 2013-14, kufuatia jeraha ya kuvunjika mguu akiwa na klabu yake ya Arsenal, na ilimchukua muda mrefu kabla ya kurejea tena uwanjani.
Baada ya msimu huu kiungo huyo atalazimika kurejea kaskazini mwa jijini London yalipo makao makuu ya klabu yake ya Arsenal, kufuatia mkataba wake wa mkopo kutarajia kufikia kikomo mwezi Juni mwaka huu.