Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kuwapatia ajira madaktari 258 na wataalamu wa Afya 11 waliopeleka maombi na kukidhi vigezo kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma.
“Kwa upande wetu sisi ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za madaktari hao ilikubalika na pande zote iwe tarehe 6 Aprili 2017 na Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili 2017, hadi tarehe ya Taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za madaktari wa Tanzania nchini Kenya,”amesema Mwalimu.
Amesema kuwa kufuatia uamuzi huo majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika Tovuti ya Wizara pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 waliopeleka maombi yao na kukidhi vigezo.
Aidha, Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka madaktari nchini Kenya.
Hata hivyo, Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dkt.Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano(500) ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya na kukubali ombi hilo.