Mlinda mlango mkongwe na nahodha wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC, Gianluigi Buffon amesema atafurahi kama timu yake itapangwa na Real Madrid au AS Monaco kwenye hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya lakini hataki kusikia kuhusu Atletico Madrid.
Juve wametinga hatua hiyo baada ya kuiondosha FC Barcelona kwa ushindi wa mabao 3-0 walioupata nyumbani kabla ya kulazimisha suluhu kwenye uwanja wa Nou Camp usiku wa kuamkia leo.
Kabla ya kupangwa kwa droo ya robo fainali Buffon aliwaambia waandishi wa habari kuwa angependa wakutane na FC Barcelona na si timu nyingine yoyote.
Droo ya nusu fainali ya michuano hiyo itapangwa kesho Ijumaa na Buffon anaamini kitendo cha Madrid na AS Monaco kuwepo katika mbio za ubingwa wa ligi za nyumbani kitawarahisishia wao (Juve) harakati zao za kufika fainali na kutwaa ubingwa huo wa Ulaya.
“Labda ni bora kukutana na Real au AS Monaco ambao watatumia nguvu nyingi kupigania ubingwa wa ligi zao, hawa hawawezi kuwa hatari kama Atletico ambao wamejihakikishia nafasi nzuri katika ligi yao na hawapo kwenye wanaowania ubingwa,” alisema Buffon akizungumza na Mediaset Premium.
Katika hatua nyingine kipa huyo anayetarajiwa kutimiza miaka 40 mwakani, amestaajabishwa na kitendo cha timu yake kutofungwa hata bao moja katika michezo miwili waliyokutana na FC Barcelona.
“Licha ya matokeo, tumekuwa bora sana, kucheza michezo miwili dhidi ya Barca bila kufungwa hata bao moja ni kitu cha kushangaza, lakini hii itatusaidia kutuongezea kujiamini tunapoingia hatua ya nusu fainali na timu bora zaidi duniani.
“Baada ya ushindi wa mabao 3-0 nyumbani nilijua tuna nafasi kubwa ya kuwaondoa Barca, lakini kiukweli sikutegemea tuje hapa Nou Camp na kutoka uwanjani bila kufungwa hata bao moja,” alimaliza Buffon.
AS Monaco wameingia katika hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwa kuifunga Borussia Dortmund mabao matatu kwa moja.
Vinara hao wa ligi ya Ufaransa wamesonga mbele kwa jumla ya mabao sita kwa matatu.