Katika maisha ya kawaida ya Watanzania tulio wengi, kwa namna moja ama nyingine umewahi kusikia au wewe binafsi kulalama kuwa pesa yako haikai au haiendi kama unavyotegemea. Hiki ni kilio cha kawaida ambacho hakitokani na kutapanya fedha bali kutojua mbinu sahihi ya kawaida tu ya kuzitumia vyema pesa ‘kidogo’ kupata matokeo makubwa.
Moja kati ya tabia ya fedha hasa hizi tunazopata watu wa kima cha chini ni kwamba huwa ni kama zinayaita matatizo au matumizi, pindi tunapokuwa nazo. Yaani mambo yanaweza kwenda tofauti na ulivyokuwa umepanga, matumizi yanaongezeka kidogo-kidogo ila unashtuka umebaki na kisalio ‘kiduchu’ au hata umefilisika kabisa. Ndio hapo kilio cha ‘mishahara haikutani’ kinazidi.
Leo tutakupa mbinu ya namna ya kubadili kidogo mtindo wako wa maisha bila kujibana bali kubana mianya ya kutumia fedha zako bila kufuata mipango uliyojiwekea.
Epuka vishawishi vya ATM, Simu Pesa:
Jitahidi mara kadhaa kukwepa kutembea na ATM au kuweka fedha nyingi kwenye simu yako ya mkononi. Chukua kiasi fulani cha fedha taslimu uliyopanga kutumia siku hiyo au wiki hiyo, ongeza na kiasi kidogo tu cha ‘dharura’. Hii ni kwa ajili ya mahitaji ya kawaida. Itakusaidia kuepuka kutumia fedha za akiba mara kwa mara pale uonapo kitu bila mpangilio kwa sababu tu unajua utaingia ATM na kuchomoa au utaivuta kutoka Simu pesa.
Itakusaidia kukwepa pia kuwapa ofa rafiki na jamaa kwa ‘mizuka’, hasa baada ya kupata kilevi. Hatusemi usiweke fedha kwenye simu, bali usiweke kiasi kikubwa kama akiba tu na kutembea nazo. Hakika utazitumia bila kupanga kama huna msimamo wa ‘bahiri’. Kumbuka kutumia ATM/ simu pesa mara kadhaa unaongeza makato ya fedha kwa huduma.
Epuka tabia za ‘nunua sasa lipa baadae’
Kampeni za ‘nunua sasa, lipa baadae’ zina msaada mkubwa kwa watu wenye mahitaji fulani kwa wakati huo lakini wanategemea kupata fedha baadae kidogo. Lakini ni hatari zaidi kwa usawa huu kwani ni rahisi kunogewa kuchukua vitu ambavyo sio vya lazima sana ukiiwaza fedha ya baadae bila kuweka akilini kuwa hiyo baadae pia itakuwa na mahitaji yake.
Jitahidi kutumia fedha kutoka kwenye mfuko uliopo sasa kama suala hilo sio la lazima sana kwa wakati huo, kama ni kiatu kizuri, kumbuka kinaweza kupatikana kizuri zaidi wakati ujao na ukakilipia kulingana na pesa itakayokuwepo kwa mazingira hayo.
Usifuje pesa yako kwenye majina ya bidhaa
Hakikisha unanua bidhaa unayoihitaji kwa gharama ambazo unaweza kuzimudu bila kufuata mkumbo wa jina la duka fulani. Usitafute jina tu kuwa umeweza kununua sehemu fulani kama fulani. Fikiria kwanza kama bidhaa hiyo haiwezi kupatikana sehemu nyingine unayoweza kufika na kupunguza gharama. Zingatia pia uhalisia wa ubora wa bidhaa husika ili isije kugeuka hasara kubwa na kukugharimu zaidi.
Andaa, pitia na ifanyie tathmini bajeti yako
“Mali bila daftari, huisha bila habari”. Hakikisha sio tu kwamba unaandaa bajeti ya matumizi yako ya mwezi, lakini pia ifanyie mapitio wakati wa matumizi na ifanyie pia tathmini kama umeitumia ipasavyo. Hii itakusaidia kuondoa matumizi yasiyo ya lazima na kujiwekea kiwango cha wastani wa matumizi yako ili kupata nafasi ya kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo na mambo mengine makubwa.
Usiogope kuahirisha
Unapaswa kufahamu kuwa kuna wakati inakulazimu kuahirisha mpango wa kufanya matumizi fulani sio kwa sababu hauna fedha inayotosha, bali matumizi ya pesa hiyo yatakupa ukata wa haraka na kilio kabla ya kupata nyingine.
Kama ni hivyo, usiogope kuahirisha mpango wako mzuri. Ni vyema ukaahirisha na kujiandaa vizuri zaidi ili uweze kumudu kufanya matumizi hayo husika bila kilio cha baadae. Kuahirisha kwa sababu za msingi ni bora kuliko kulazimisha kwa shida ya kipindi.
Kumbuka, hakuna fedha nyingi bila fedha ndogo, unapotumia fedha kwa matumizi unayoyaita madogo tu fahamu kuwa unabandua sehemu ya gogo lako. Hivyo, halitakuwa kama ulivyotaka kwa muda husika.
Ukitoa shilingi moja kwenye milioni moja haitaitwa tena milioni moja. Kuwa na nidhamu ya fedha, ni siri ya mafanikio hasa kwenye kipindi kigumu cha maisha.
Hii ni sehemu tu ya unayopaswa kuyafanya kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.