Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta leo amevionya vikundi au watu wanaopanga kufanya vurugu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika mwezi Agosti kuwa hatawavumilia.
Kupitia taarifa yake kwa wananchi wa Kenya, Rais Kenyatta amesema kuwa serikali na chama chake havitawavumilia watu hao na kwamba mgombea yeyote atakayebainika kuhusika katika vurugu atakuwa amejiondolea sifa za kuwa mgombea na anaweza kushitakiwa mahakamani.
“Vurugu na machafuko ambayo yameonekana katika ngazi za chini hayatavumilika. Utamaduni wa vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi ni lazima usikubalike,” alisema Rais Kenyatta.
Tamko hilo la Rais Kenyatta limekuja wakati ambapo tayari kuna wanasiasa wawili wanaowania nafasi za ubunge wanaendelea kupewa matibabu hospitalini kutokana na majeraha waliyoyapata kwenye vurugu za mchakato wa uchaguzi huo.
Kenya inazikumbuka na kulaani vurugu za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200 na zaidi ya watu 500,000 kukosa makazi.