Sakata la Richmond limechukua sura mpya Bungeni mara baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema) kumtuhumu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kuwa hakutenda haki wakati alipokuwa akishughulikia suala hilo.
Wabunge hao kwa pamoja wamemtuhumu Waziri huyo kwa kusema kuwa wakati akiongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza Kamapuni tata ya ufuaji umeme kuwa haikumtendea haki aliyekuwa Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Edward Lowassa kwakuwa hakumpatia muda wa kumhoji kitu ambacho kilipelekea kujiuzuru.
Aidha, akijibu hoja hizo Waziri Mwakyembe amesema kuwa kama kuna mtu yeyote ambaye ni jasiri wa kurudisha suala hilo bungeni afanye hivyo ili aweze kulishughulikia kikamilifu na kuamaliza utata.
“Naomba nimalizie kwamba, mimi naahidi kwamba siku ambayo kuna mmoja atakuwa jasiri wa kuleta suala la Richmond hapa, nitamuomba Rais anipumzishe Uwaziri ili niweze kuishughulikia kesi hiyo kikamilifu,”amesema Mwakyembe.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Wapinzani watakuwa na kazi kubwa sana kuweza kumsafisha mtu ambaye alikuwa ni mtuhumiwa kwa kuwa wengi hawajui undani wa suala hilo.