Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa Waalimu wanaoutoa katika kupandisha kiwango cha Sekta ya Elimu hapa Nchini.
Ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu hatua za malipo na malimbikizo ya madeni kwa waalimu.
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2014 hadi kufikia mwaka 2016 ufaulu umeongeka katika ngazi zote kitu ambacho kinaashiria kupanda kwa kiwango cha elimu.
“Tunaambiwa elimu inashuka, sijui wanatumia takwimu gani, lakini tunachoweza kujua inapanda au inashuka ni matokeo ya mitihani, kama kipo kigezo kingine labda ni baadaye,”amesema Simbachawene.
Aidha,ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua kulipa malimbikizo ya madeni yao, lakini pia imeanzisha posho maalumu ya madaraka kwa waalimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu huku ikiimarisha na kutengeneza mazingira rafiki ya kufundishia.
Hata hivyo, amewataka waalimu nchini kutojazwa upepo kwani anaamini Serikali inatambua mchango wao na inachukua hatua stahiki kulipa madeni yao na kuongeza kuwa tayari wameshalipa madeni ya shilingi bilioni 3 katika Mikoa yote.